Guterres asisitiza udharura wa kusitishwa vita vya Ethiopia
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba mapigano ya kijeshi nchini Ethiopia hayataleta amani wala uthabiti wa kudumu katika nchi hiyo ya Afrika.
Kupitia taarifa aliyotoa jana Jumanne, Guterres amezitaka pande zote zinazopigana nchini humo kuhitimisha mapigano mara moja. Ametaka kipaumbele kitolewe kwa usalama wa raia na kuruhusiwa misaada ya kibinadamu kufikishiwa wahitaji bila kuwekwa vizuizi katika shughuli za mashirika ya ufikishaji misaada ya kibinadamu.
Vilevile Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka wafanyakazi wote wa umoja huo waliokamatwa kwa tuhuma mbalimbali zisizothibitishwa waachiliwe huru mara moja.
Antonio Guterres amebainisha wasiwasi wake kuhusiana na ripoti zinazothibitisha kukamatwa kinyume cha sheria baadhi ya raia wa Ethiopia na kuonya kuwa huenda suala hilo likazidisha migawanyiko nchini humo.
Serikali ya Ethiopia ilitoa amri ya kushambuliwa eneo la Tigray lililo kaskazini mwa nchi baada ya kuwatuhumu wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF) kuwa walishambulia jeshi la serikali katika eneo hilo. Vita hivyo vimeutia wasiwasi mkubwa Umoja wa Mataifa.
Vita vya kaskazini mwa Ethiopia vimepelekea watu karibu milioni mbili kuwa wakimbizi na kuwafanya wengine zaidi ya laki nne kukabiliwa na baa la njaa.
Juhudi zote za upatanishi ambazo zimekuwa zikifanywa na taasisi za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika AU zimepuuzwa na kukataliwa na pande zote mbili zinazoshiriki katika vita hivyo.