Mripuko wa homa ya manjano waua watu 25 nchini Ghana
Mripuko wa homa ya manjano umesababisha vifo vya watu wasiopungua 25 nchini Ghana.
Hayo yameripotiwa na Dakta Patrick Kuma-Aboagye, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afya ya Ghana na kuongeza kuwa, watu wengine 18 wamelazwa hospitalini baada ya kugunduliwa kuwa wanaugua maradhi hayo.
Amesema mripuko huo umeshuhudiwa katika majimbo ya Savannah na Upper West. Dakta Kuma-Aboagye amesema mripuko huo ulianzia katika eneo la Savannah lakini hivi sasa ugonjwa huo umeenea hadi katika wilaya ya Mashariki katika jimbo la Upper West.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Ghana, watu zaidi ya 43,615 walikuwa wamepigwa chanjo ya kupambana na ugonjwa huo katika eneo la Savannah kufikia Novemba 15 mwaka huu.

Kwa mujibu wa tafiti za kisayansi kuhusu ugonjwa wa homa ya manjano, binadamu anapata maradhi hayo baada ya kuumwa na mbu mwenye virusi. Mbu hao wako katika sehemu za joto, barani Afrika na Amerika ya Latini.
Ikiwa mtu ataambukizwa virusi vya ugonjwa huo, ini lake pamoja na viungo vingine vya ndani vinaweza kudhurika na kusababisha kifo.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kuwa, asilimia 90 ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa homa ya manjano vinatokea katika bara la Afrika.