Sep 18, 2024 11:26 UTC
  • WHO: Vifaru vya Israel vinawashambulia wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa vifaru vya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel vimewashambulia wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu huko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza ili kuwazuia kutoa misaada kwa wakimbizi na majeruhi wa Kipalestina.

Katika kipindi cha miezi 11 iliyopita, utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina na kutumia silaha zilizopigwa marufuku kushambulia misafara ya misaada ya kibinadamu na wafanyakazi wa huduma mbalimbali lengo kuu likiwa ni kuzidisha hali mbaya ya wakimbizi wa Kipalestina. 

Shirika la habari la Mehr limeripoti kuwa, Tedros Adhanom Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ameandika kuhusu suala hilo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba: Jumamosi iliyopita wakati msafara wa misaada ya WHO ulipokuwa umevuka kituo cha upekuzi kutokea kaskazini mwa Gaza ghafla ulikabiliwa na vifaru viwili vya jeshi la Israel. 

Tedros Adhanom, Mkukrugenzi Mkuu wa WHO 

Adhanom ameendelea kusema kuwa: Vifaru hivyo vya Israel viliufyatulia risasi msafara wa misaada wa WHO na kwa bahati nzuri hakuna mtu aliyedhurika. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani amesema kuwa, pamja na hayo kitendo hicho cha jeshi la Israel hakikubaliki. 

Wakati huo huo, Sigrid Kaag, Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu na Ujenzi Mpya wa Ukanda katika Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa hakuna mahali salama huko Gaza na kwamba usitishaji vita unapasa kufikiwa haraka iwezekanavyo. 

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, ubinadamu upo hatarini na kwamba Wapalestina zaidi ya elfu 41 wameuawa shahidi katika Ukanda wa Gaza.  

Tags