Upinzani dhidi ya wanajeshi wa Ufaransa waongezeka Niger, Burkina Faso
(last modified Sun, 28 Nov 2021 02:51:41 GMT )
Nov 28, 2021 02:51 UTC
  • Upinzani dhidi ya wanajeshi wa Ufaransa waongezeka Niger, Burkina Faso

Asasi za kitaifa za Niger zimeendelea na harakati kama za wananchi wa Burkina Faso za kufanya maandamano ya kupinga kuwepo wanajeshi wa Ufaransa katika nchi hizo.

Shirika la habari la IRNA lilitangaza jana kuwa, msafara wa wanajeshi wa mkoloni Mfaransa ambao umeingia Niger kutokea Burkina Faso, umekumbwa na maandamano na upinzani mkubwa kutoka kwa harakati ya "Let's Turn the Page (TLP)" ambayo inaundwa na asasi zaidi ya 200 za kiraia za Niger.  Harakati hiyo imetoa mwito wa kufanyika maandamano makubwa ya amani tarehe 5 mwezi ujao wa Disemba ili kutangaza upinzani wao wa kuweko wanajeshi wa mkoloni Mfaransa huko Niger.

Msafara wa kijeshi wa Ufaransa ambao unaelekea nchini Mali, uliingia katika ardhi ya Niger juzi Ijumaa, baada ya kuhangaika wiki nzima katika mji wa Kaya nchini Burkina Faso kutokana na wananchi kuufungia njia. Msafara huo ulifungiwa njia na wananchi katika miji yote uliopita huko Burkina Faso.

Wananchi hawawataki wakoloni ving'ang'anizi wa Ufaransa

 

Wiki iliyopita waandamanaji wenye hasira nchini Burkina Faso waliufungia njia msafara huo wa kijeshi wa mkoloni Ufaransa wakati ulipokuwa unaelekea katika nchi jirani ya Niger ikiwa ni kulalalamikia namna mkoloni huyo mkongwe wa Ulaya alivyoshindwa kuwadhaminia usalama wao licha ya kutuma wanajeshi wake katika eneo hilo kwa miaka mingi sasa.

Mamia ya watu wenye hasira walimiminika kwenye njia ulipokuwa unapita msafara wa magari ya wanajeshi wa Ufaransa katika mji wa Kaya. Mmoja wa waandamanaji hao alikuwa amebeba bango lenye maneno yasemayo: "Kaya inasema, wanajeshi wa Ufaransa rudini kwenu." Mmoja wa waandamanaji alinukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema: "Tumewataka wanajeshi wa Ufaransa wafungue magari yao tuone yana nini ndani."

Tags