Kuendelea mgogoro wa kisiasa nchini Sudan
Licha ya kupita wiki kadhaa tokea aliporejea madarakani Abdalla Hamdok kama waziri mkuu wa Sudan, na jeshi la nchi hiyo kuafiki aunde serikali isiyo ya kijeshi lakini mgogoro wa kisiasa bado haujamalizika, kwani wananchi wanaendeleza maandamano mitaani.
Aghalabu ya wananchi wa Sudan wanaendelea kupinga utawala wa kijeshi na wanaamini serikali ya sasa ni matunda na matokeo ya kuelegeza msimamo mbele ya matakwa ya wanajeshi. Kwa msingi huo vyama vya upinzani vinasisitiza kuendelezwa maandamano ya kuiangusha serikali ya sasa.
Kuhusiana na nukta hiyo maelfu ya watu wamekuwa wakiandamana katika mji mkuu, Khartoum na miji mingine ya Sudan. Waandamanaji wamekuwa wakikabiliana na askari ambao wamekuwa wakijaribu kuzima maandamano na watu wengi wamejeruhiwa katika ghasi zilizoibuka. Mgogoro wa sasa wa Sudan ulishadidi Oktoba 25 wakati jeshi lilipomkamata waziri mkuu Abdulla Hamdok na kumpeleka kusikojulikana na kisha wanajeshi wakatangaza kutwaa madaraka ya nchi.
Maandamano ya wananchi hatimaye yalimlazimu kingozi wa kijeshi wa Sudan Abdulfattah al Burhan kufikia mapatano na Hamdok na hivyo akarejea katika nafasi yake ya waziri mkuu.
Mapatano hayo ya kisiasa yalifikiwa kwa shabaha ya kuwatuliza waandamanaji lakini inaonekana hayakufanikiwa kufikia malengo yake ya kusitisha malalamiko ya wananchi. Vyama vya kisiasa Sudan zinasema maandamanao ya sasa yanafanyika katika fremu ya malengo ya umoja wa kitaifa na kuondoa utawala wa sasa kijeshi. Waandamanaji wanasisitiza kuwa, wataendeleza maandamano hayo hadi pale wanajeshi watakapoondoka madarakani kikamilifu na uchaguzi uitishwe.
Muungano wa Jumuiya za Wanataaluma umetangaza kuwa, maandamano yataendelea hadi pale utawala wa kijeshi utakapoondolewa na serikali ya raia kuingia madarakani.
Katika maandamano ya hivi karibuni yaliyofanyika Jumatatu malaki ya watu walijitokeza na kusisitiza kuwa lazima utawala wa kijeshi uondoke na madaraka yakabidhiwe kwa viongozi wa kiraia.
Halikadhalika Kamati ya Haki za Binadamu imetangaza kuwa inatayarisha waraka mpya wa kisiasa kwa ushirikiano na vyama kadhaa vya kisiasa. Ingawa si vyama vyote vilivyotia saini waraka huu lakini umeungwa mkono na vyama vingi nchini Sudan.
Alaa kulli hal, mgogoro wa Sudan sasa umeingia katika awamu hatari zaidi. Si tu kwamba kumeshadidi hitilafu baina ya wanajeshi na pia baina ya vyama vya kisiasa bali pia mizozo na mivutano imeshadidi zaidi baina makundi mbalimbali nchini humo.
Mohammad Hasb Al Rasul, msomo wa Sudan anasema kuhus nukta hiyo kwamba: "Mustakabali wa Sudan uko hatarini na kuna hofu kuwa nchi hii inaelekea kusikojulikana au itatumbukia katika mgogoro na machafuko, na hilo litakuwa na taathira hasi kwa usalama na ulitulivu wa nchi."
Hii ni katika hali ambayo uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya Sudan pia ungali unashuhudiwa katika uga wa kisiasa ya nchi hiyo.
Wakati huo huo matamshi ya wakuu wa Marekani, Ulaya na uingiliaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel ni miongoni mwa mambo ambayo yamepelekea kushadidi mgogoro wa Sudan. Kwa mfano tu Jeffrey Feltman Mjumbe Maalumu wa Marekani katika eneo la Pembe ya Afrika amesisitiza ulazima wa kuwepo ushirikiano baina ya wanajeshi na raia ili uchaguzi wa Sudan ufanyike, na amedai kuwa taifa la Sudan limepoteza matumaini ya kuelekea katika demokrasia.
Dakta Mohammad Uthman mkurugenzi wa Kituo Utafiti cha Maarifat Riyadh amesema: "Matamshi ya Feltman ni ya kutiliwa shaka na ni thibitisho kuwa lengo lake ni kutimiz matakwa ya Ikulu ya White House nchini Sudan.