Serikali ya Tanzania yawataka raia wachukue tahadhari ya magonjwa ya kuambukiza
Wizara ya Afya ya Tanzania imewataka raia kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya kuambukiza, wakati huu hospitali nyingi nchini humo, zikiripoti ongezeko la wagonjwa wanaougua mafua, kifua na maumivu ya viungo.
Katibu Mkuu wa wizara ya afya nchini humo, Profesa Abel Makubi, amesema, wanafuatilia mwenendo wa kusambaa kwa mafua na homa na kwamba wizara hiyo itaendelea kutoa taarifa mara kwa mara.
Kauli yake imekuja wakati huu baadhi ya hospitali nchini Tanzania zikiripoti kupokea idadi kubwa ya watu wenye mafua, homa na maumivu ya mwili, ambapo wataalamu wanasema, huenda inatokana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayoshuhudiwa nchini humo.

Baadhi ya raia kupitia mitandao ya kijamii wamedai kusumbuliwa na mafua makali, hali ambayo imeibua hofu kuwa huenda ni maambukizi ya virusi vya Corona, ukizingatia kilichotokea kuanzia mwishoni mwa mwaka jana hadi mwanzoni mwa mwaka huu, ambapo watu kadhaa waliripotiwa kupoteza maisha nchini humo kutokana na virusi hivyo.
Hata hivyo hali hiyo haijaripotiwa nchini Tanzania pekee kwani katika nchi jirani ya Kenya wananchi wametumia mitandao ya kijamii kuhoji juu ya kusambaa mafua wakati huu nchi hiyo ikirekodi uwepo wa wagonjwa wa walioambukizwa spishi mpya ya kirusi cha corona ya Omicron.../