Waasi wa Tigray warudi nyuma na kuondoka maeneo waliyokuwa wakiyadhibiti
Mkuu wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) ametangaza kuwa, wapiganaji wa harakati hiyo wamerudi nyumana kuondoka katika maeneo yote nje ya eneo la Tigray huko kaskazini mwa Ethiopia ikiwa ni katika kujibu maombi ya kimataifa na kutoa fursa ya kurejesha amani katika eneo hilo.
Mkuu wa harakati ya TPL ameeleza kuwa, wanauomba Umoja wa Mataifa uweke marufuku ya ndege kuruka katika eneo la Tigray na kuzuia kuingizwa silaha nchini Ethiopia na Eritrea. Waasi wa eneo la Tigray ambao katika miezi kadhaa iliyopita walisonga mbele katika maeneo jirani ya Amhara na Afar hivi sasa wanaondoka kuelekea katika maeneo yao ili kufungua njia kwa ajili ya misaada ya kibinadamu.
Waasi wa TPLF wanasema kuwa, wameamua kufungua mlango ili misaada ya kibinadamu iwafikie raia.
Ethiopia katika miezi ya karibuni imeshuhudia matukio mengi ikiwa ni pamoja na mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo na waasi wa harakati ya TPLF katika eneo lal Tigray.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Novemba 4 mwaka jana alitoa amri ya kushambuliwa eneo la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo baada ya kuwatuhumu waasi wa TPLF kuwa wamevishambulizi vikosi vya jeshi la nchi hiyo.
Mapigano huko Tigray hadi sasa yamesababisha watu karibu milioni mbili kuwa wakimbizi na maelfu ya wengine pia kukabiliwa na njaa na ukosefu wa chakula.