Ethiopia: Hatuna nia ya kuwashambulia waasi wa Tigray
Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa, haina nia ya kuendeleza mashambulizi dhidi ya waasi wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF).
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Redwan Hussein amesema katika mkutano wake na mabalozi wa nchi za kigeni mjini Addis Ababa kwamba, serikali ya Ethiopia haikusudii kuendeleza mashambulizi dhidi ya vikosi vya kundi la Tigris People's Liberation Front lakini inataka kuhakikisha kuwa, waasi wa Tigray hawana tena uwezo wa kupanga upya operesheni za mashambulizi katika maeneo yanayodhibitiwa na jeshi la Ethiopia.
Akizungumzia hali ya sasa ya Ethiopia, Redwan Hussein ameashiria kikao maalumu cha hivi karibuni cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuhusu Ethiopia na amekosoa kuundwa kwa jopokazi la kimataifa litakalochunguza masuala ya haki za binadamu nchini humo akisema ni jambo lisilokubalika.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia ameongeza kuwa, ilikuwa jambo la mantiki zaidi kwa Kamisheni Kuu ya Kuhudumia Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa (UNHCR) na Tume ya Umoja wa Ulaya ya Haki za Binadamu kuanzisha uchunguzi kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na waasi wa Tigray katika maeneo ya Amhara na Afar.
Itakumbukwa kuwa, Ijumaa iliyopita Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa lilipiga kura ya kutuma wachunguzi wa kimataifa katika taifa hilo la pili kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika huku kukiwa na onyo la kutokea ukatili mkubwa, hatua iliyopingwa na Addis Ababa.