Katibu Mkuu wa UN alitaka jeshi Sudan liache kushambulia waandamanaji
(last modified Tue, 04 Jan 2022 12:46:47 GMT )
Jan 04, 2022 12:46 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN alitaka jeshi Sudan liache kushambulia waandamanaji

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amevisihi vikosi vya usalama nchini Sudan vizingatie wajibu wao juu ya uhuru na haki ya kuandamana na kujieleza, kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 25 mwezi Oktoba mwaka uliopita wa 2021.

Antonio Guterres ametoa mwito huo, huku ghasia na maandamanao yakiendelea kuripotiwa nchini Sudan sambamba na hatua ya Waziri Mkuu Abdalla Hamdok ya kuamua kujiuzulu,

Guterres ameeleza katika taarifa kwamba, anatambua hatua ya kujiuzulu Bwana Hamdok, lakini anasikitika kuona kuwa, bado hakuna mwelekeo wa maelewano ya kisiasa licha ya hali kuzidi kuwa mbaya nchini humo.

Baada ya kukamatwa na kuwekwa ndani wakati jeshi lilipotwaa madaraka tarehe 25 mwezi Oktoba mwaka jana, sambamba na maafisa wengine waandamizi na wanaharakati wa kisiasa, Hamdok alirejeshwa madarakani kufuatia makubaliano kati yake na jeshi ya kugawana madaraka.

Hata hivyo vyombo vya habari viliripoti jana kuwa waziri mkuu Hamdok amejiuzulu baada ya siku nzima ya maandamano katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum.

Antonio Guterres

Taarifa ya Katibu Mkuu wa UN imesisitiza: "chonde chonde wadau wote waendelee kushiriki katika mazungumzo sahihi ili kufikia suluhu jumuishi, ya amani na ya kudumu.”

Halikadhalika, amekumbusha kuwa matamanio ya wananchi wa Sudan ya kuwa na kipindi cha mpito kitakachowafikisha katika mazingira ya demokrasia bora, ni muhimu zaidi.

Guterres amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake uko tayari kufanikisha mwelekeo huo.

Wakati huohuo, Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kusimamia kipindi cha mpito nchini Sudan UNITAMS Volker Perthes naye amesema, anaheshimu uamuzi wa Bwana Hamdok kujiuzulu na kupongeza mafanikio yaliyofikiwa chini ya uongozi wake sambamba na mafanikio aliyofikia wakati wa awamu ya kwanza ya kipindi cha mpito.

Sambamba na kauli hiyo, Perthes ametoa indhari akisema, “bado nina wasiwasi mkubwa juu ya janga la kisiasa linaloendelea, kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 25 mwezi Oktoba mwaka jana wa 2021, ambalo linahatarisha maendeleo yaliyofikiwa tangu mapinduzi ya mwezi Desemba 2019."

Aidha amesema, anatiwa wasiwasi na idadi ya raia wanaouawa na kujeruhiwa katika maandamano yanayoendelea hivi sasa nchini Sudan.../

Tags