Afrika CDC: Kuzifunga nchi hakuna manufaa katika kudhibiti Corona
Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika CDC kimesema kuzifunga nchi na kuweka sheria za kutotoka nje si moja ya njia bora zaidi za kukabiliana na msambao wa virusi vya Corona.
Mkuu wa kituo hicho cha Umoja wa Afrika, John Nkengasong, amesema enzi za kutumia njia hizo zimepitwa na wakati, na kinachotakiwa kufanywa ni kuangalia kwa makini namna nchi zinavyotumia mfumo wa afya ya umma na kanuni za kijamii za kudhibiti msambao wa virusi hivyo hatarishi.
Aidha kwa mara nyingine tena, Nkengasong amewakosoa vikali viongozi wa dunia kwa kushindwa kutekeleza ahadi zao kuhusu mgao wa chanjo za Corona, akisisitiza kuwa nchi tajiri duniani zinajirundikia chanjo bila kuzijali nchi maskini.
Amesema mwenendo wa kinyonga wa kuwachanja wananchi wa nchi za Afrika huenda ukapelekea ugonjwa wa Corona ukasalia kuwa janga lisilokwisha barani humo.
Hadi hivi sasa ni chini ya asilimia 10 ya jamii yote ya Waafrika bilioni 1.3 waliopata chanjo kamili ya ugonjwa wa Covid-19. Aidha ni nchi saba tu za Kiafrika zilizofanikiwa kufikia lengo la Shirika la Afya Duniani (WHO), la kuchanja asilimia 40 ya watu wake kufikia mwishoni mwa mwaka uliomalizika 2021.
Kwa mujibu wa takwimu za Afrika CDC, watu 9,756,457 wameambukizwa Covid-19 barani Afrika kufikia sasa, huku idadi ya walioaga dunia kwa maradhi hayo hadi sasa barani humo ikiwa ni 228,856.