UN yasitisha misaada ya kibinadamu katika eneo la Tigray, Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i79026-un_yasitisha_misaada_ya_kibinadamu_katika_eneo_la_tigray_ethiopia
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa umesitisha operesheni za kupeleka misaada ya kibinadamu katika jimbo la Tigray baada ya ndege za kijeshi za Ethiopia kushambulia kambi ya wakimbizi katika eneo hilo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 10, 2022 03:10 UTC
  • UN yasitisha misaada ya kibinadamu katika eneo la Tigray, Ethiopia

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa umesitisha operesheni za kupeleka misaada ya kibinadamu katika jimbo la Tigray baada ya ndege za kijeshi za Ethiopia kushambulia kambi ya wakimbizi katika eneo hilo.

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imesema kuwa, mashirika ya misaada ya kibinadamu ya umoja huo yamesitisha shughuli zao huko Tigray baada ya mashambulizi ya anga ya jeshi la Ethiopia yaliyolenga kambi ya wakimbizi na kuua makumi ya raia.

Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya  Umoja wa Mataifa (OCHA) imetangaza kuwa, watu 56 wameuawa na wengine 30 wamejeruhiwa katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao kwenye mji wa Dedebit, kaskazini-magharibi mwa eneo la karibu na mpaka na Eritrea. 

Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema kuwa idadi ya watu waliouawa katika shambulio hilo imedhibitishwa na maafisa wa utawala wa eneo hilo.

Wakimbizi wa Tigray

Disemba 30 mwaka jana pia Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa iliripoti kuwa, makumi ya raia wameuawa katika mashambulizi ya anga  kusini mwa eneo la Tigray. Umoja wa Mataifa uliyataja mauaji hayo ya raia kuwa mashambulizi makali zaidi kuwahi kuripotiwa tangu mwezi Oktoba mwaka jana.