Usalama waimarishwa Khartoum Sudan; maandamano mengine yatarajiwa
(last modified Wed, 12 Jan 2022 08:15:49 GMT )
Jan 12, 2022 08:15 UTC
  • Usalama waimarishwa Khartoum Sudan; maandamano mengine yatarajiwa

Serikali ya kijeshi ya Sudan ambayo katika siku za karibuni imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa za malalalamiko na maandamano ya wananchi, imeimarisha usalama katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum.

Hatua hiyo ya kuimarisha usalama na kutuma askari wengi katika mitaa mbalimbali ya mji mkuu Khartoum inakuja baada ya kuweko taarifa kwamba, wananchi wa Sudan leo pia wanatarajiwa kufanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi hiyo hususan Khartoum.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, tangazo la kufanyika maandamano hayo leo ndilo lililowafanya majenerali wa jeshi wanaoongoza nchini Sudan kuchukua hatua za kuimarisha usalama kwa ajili ya kukabiliana na waandamanaji hao.

Maandamano ya wananchi wa Sudan

 

Mgogoro wa Sudan ulishadidi zaidi Oktoba mwaka jana baada ya wanajeshi kutwaa madaraka ya nchi. Kushika hatamu za uongozi wanajeshi, kuliibua hasira na ghadhabu za wananchi wa Sudan. Wananchi wa Sudan wanaamini kuwa, kuweko madarakani wanajeshi ni kinyume kabisa na malengo ya mapinduzi yao yaliyopelekea kuondolewa madarakani Omar al-Bashir. Kilio na takwa kuu la wananchi wa Sudan ni jeshi kuachia ngazi na kisha kuingia madarakani serikali ya kiraia na ya kidemokrasia.

Licha ya maandamano ya wananchi, lakini majenerali wa jeshi nchini Sudan wanaoongozwa na Abdel-Fatah al-Burhan hawako tayari kuachia uongozi na wamekuwa wakitumia mkono wa chuma kukandamiza maandamano ya wananchi ambayo yamekuwa yakishadidi siku baada ya siku.

Tags