UN: Hujuma za anga Tigray zimeua raia 108 wa Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i79210-un_hujuma_za_anga_tigray_zimeua_raia_108_wa_ethiopia
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, kwa akali raia 108 wameuawa tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari hadi sasa, katika mashambulizi ya anga katika eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 14, 2022 21:19 UTC
  • UN: Hujuma za anga Tigray zimeua raia 108 wa Ethiopia

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, kwa akali raia 108 wameuawa tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari hadi sasa, katika mashambulizi ya anga katika eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia.

Liz Throssell, msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN aliwaambia waandishi wa habari jana Ijumaa mjini Geneva kuwa, mbali na raia 108 kuuawa katika hujuma hizo za anga za jeshi la serikali ya Ethiopia ndani ya mwezi huu, lakini wengine 75 wamejeruhiwa.

Ameashiria shambulio la anga la Ijumaa ya wiki iliyopita, lililolenga mji wa Dedebit, kaskazini-magharibi mwa eneo la karibu na mpaka na Eritrea na kusema kuwa, hujuma hiyo ilisababisha vifo vya watu 56 na kujeruhi wengine 30 wakiwemo watoto.

Afisa huyo wa UN amezitaka mamlaka za Ethiopia na waitifaki wao kuhakikisha kuwa raia wanalindwa katika operesheni hizo, na kutilia maanani wajibu wao chini ya sheria za kimataifa.

Mapigano eneo la Tigray

Itakumbukwa kuwa, Disemba 30 mwaka jana, Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) iliripoti kuwa, makumi ya raia wameuawa katika mashambulizi mengine ya anga huko kusini mwa eneo la Tigray.

Makabiliano na mzozo mkubwa unaendelea kushuhudiwa kwa miezi 14 sasa kati ya serikali ya serikali ya Ethiopia na kundi la waasi wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF).