Wapinzani Sudan watoa wito wa kufanyika uasi wa kijamii
Muungano wa kisiasa wa Uhuru wa Mabadiliko nchini Sudan umetoa taarifa ukiwahimzia wananchi kufanya uasi wa kijamii.
Taarifa iliyotolewa jana na muungano huo katika kampeni ya kuendeleza malalamiko ya wananchi dhidi ya hatua za kamanda wa jeshi la Sudan, Abdel Fattaha al Burhan imetoa wito wa kufanyika uasi wa kijamii nchini Sudan kwa muda wa siku mbili.
Muungano wa Uhuru na Mabadiliko umesema kuwa serikali ya wafanyamapinduzi inaendelea kuwasaliti wananchi waliojitosa mitaani kwa ajili ya kupigania uhuru na utukufu wao na inakabiliana nao kwa risasi na mtutu wa bunduki.
Jumuiya ya Madaktari wa Sudan iliripoti jana kuwa, polisi wa nchi hiyo wamewaua watu saba katika maandamano mapya dhidi ya utawala wa kijeshi nchini humo.
Jumuiya hiyo imeeleza kuwa hadi sasa watu 71 wameuawa katika ghasia na mapigano kati ya askari usalama na waandamanaji mjini Khartoum na katika miji mingine ya Sudan tangu baada ya mapinduzi ya Oktoba 25 mwaka jana.
Umoja wa Mataifa pia umetangaza kuwa, una wasiwasi kutokana na machafuko na umwagaji damu unaoendelea huko Sudan na umetahadharisha juu ya uwezekano wa kushuhudiwa maafa zaidi ya binadamu nchini humo.