Ujumbe wa ECOWAS wawasili Burkina Faso na kukutana wanajeshi wafanyamapinduzi
Ujumbe wa wakuu wa majeshi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS umewasili nchini Burkina Faso na kukutana na kufanya mazungumzo na wajumbe wa baraza la wanajeshi walioongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini humo.
Mkutano huo umefanyika baada ya viongozi wa ECOWAS kuchukua uamuzi wa kusimamisha uanachama wa Burkina Faso katika jumuiya hiyo.
Ujumbe huo wa wakuu wa majeshi ya nchi wanachama wa ECOWAS uliowasili mjini Ouagadougou hapo jana ulitazamiwa kubakia nchini humo hadi leo.
Imeelezwa kuwa, lengo la safari ya ujumbe huo wa Ecowas huko Burkina Faso, unaojumuisha wakuu wa majeshi ya Benin, Togo na Ghana, ni kuchunguza hali ya mambo na mazingira yalivyo kabla ya kuelekea nchini humo ujumbe mwingine wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama, ambao unatazamiwa kuwasili mjini Ouagadougou kesho Jumatatu na kufanya mazungumzo na baraza tawala la kijeshi.
Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magahribi watakutana Februari 3 katika mji mku wa Ghana, Accra ili kutathmini matokeo ya kazi itakayofanywa na jumbe zilizotumwa nchini Burkina Faso na kuona kama nchi hiyo iwekewe vikwazo pia mbali na kusimamishwa uanachama wake au la.
Watawala wapya wa kijeshi nchini Burkina Faso wametetea uamuzi wao wa kufanya mapinbduzi kwa kudai kwamba Rais Roch Marc Christian Kabore wa nchi hiyo ameshindwa kuzima machafuko ambayo yamepelekea maelfu ya watu kuuawa wakati wa utawala wake.
Mbali na Burkina Faso, ndani ya kipindi cha miezi 18 sasa, nchi nyingine mbili za Guinea na Mali, ambazo nazo pia ni wanachama wa ECOWAS zimeshuhudia mapinduzi ya kijeshi ambayo yamelaaniwa kikanda na kimataifa.../