Feb 07, 2022 12:40 UTC
  • Kimbunga Batsirai chaikumba Madagascar, 10 wauawa na 48,000 wameyahama makazi yao

Watu wasiopungua 10 wameaga dunia na karibu 48,000 wamekimbia makazi yao kutoka na kimbunga Batsirai, ambacho kimekikumba kisiwa hicho kilichoko kilomita 400 kutoka pwani ya Mashariki ya Afrika.

Vyombo vya habari vya Madagascar vimetangaza kuwa, baadhi ya watu wameuawa baada ya nyumba zao kuporomoka katika mji wa Ambalavao, takriban maili 286 kusini mwa mji mkuu, Antananarivo. 

Kimbunga Batsirai kilifika eneo la Mananjary, kikiwa na upepo unaokwenda kwa kasi ya maili 103 kwa saa, na kung'oa miti, kuharibu majengo na kuwafanya maelfu ya watu kukosa makazi yao.

Ofisi ya Taifa ya Hali ya Hewa ya Madagascar imetangaza kuwa mvua kubwa itasababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Jumamosi iliyopita Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) lilitabiri kuwa kimbunga Batsirai kinatazamiwa kusababisha upepo mkali na mvua kubwa katika maeneo ya pwani ya Madagascar.

Kimbunga Batsirai kiimeikumba Madagascar chini ya wiki mbili baada ya kimbunga kingine cha kitropiki kwa jina la Ana kusababisha vifo vya watu 58 huku wengine zaidi ya 130,000 wakipoteza makazi yao kisiwani Madagascar.

Madagascar imekuwa ikikumbwa na vimbunga mara kwa mara ambavyo mbali na kusababisha maafa na kupelekea malaki ya watu kuachwa bila makazi, lakini huathiri pia miundomsingi na mifumo ya mawasiliano.

Tags