6 wauawa, 13 wajeruhiwa katika shambulio la bomu Somalia
Watu wasiopungua sita wameuawa katika mripuko wa bomu uliotokea katika makutano ya barabara yenye shughuli nyingi ya El Gaab katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Msemaji wa Polisi ya Somalia mjini Mogadishu, Abdifatah Aden Hassan, amesema watu wengine 13 wamejeruhiwa katika shambulio hilo lililofanywa na gaidi aliyekuwa amejifunga mada za miripuko kiunoni.
Amesema gaidi huyo alikusudia kuulenga msafara wa magari yaliyokuwa yamewabeba wapiga kura ambao walikuwa wanarejea nyumbani kutoka kituo cha kupigia kura mjini hapo, lakini akanoa.
Mashuhuda wameliambia shirika la habari la Xinhua kuwa, sauti kubwa ya mripuko ilisikika katika eneo hilo asubuhi mwendo wa saa nne na nusu kwa saa za nchi hiyo, na kusababisha taharuki na hofu kubwa.
Duru za hospitali zinasema yumkini idadi ya wahanga wa hujuma hiyo ikaongezeka, kutokana na hali ya mbaya ya majeruhi wa shambulio hilo linalosadikika kuwa la kigaidi.
Hadi tunaenda mitamboni, hakuna genge lililokuwa limetangaza kuhusika na shambulio hilo la jana Alkhamisi jijini Mogadishu. Hata hivyo wapiganaji wa kundi la wanamgambo wa al Shabab na mtandao wa al Qaida wanaotekeleza hujuma mbalimbali kwa shabaha ya kuing'oa madarakani serikali ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, wamekuwa wakidai kuhusika na mashambulio mbalimbali huko Somalia na nje ya nchi hiyo.