Burhan apongeza 'uhusiano wa kijasusi' wa Sudan na Israel
(last modified Sun, 13 Feb 2022 12:37:12 GMT )
Feb 13, 2022 12:37 UTC
  • Burhan apongeza 'uhusiano wa kijasusi' wa Sudan na Israel

Mkuu wa Jeshi la Sudan, Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan amejitokeza hadharani na kutetea kitendo chake cha kiafriti, cha kushinikiza kuboresha uhusiano wa kawaida wa nchi hiyo na utawala haramu wa Israel.

Katika mahojiano na runinga ya taifa jana jioni, Burhan amedai kuwa, ni halali kwa vyombo vya usalama na intelijensia vya Sudan kuwa na uhusiano wa karibu na Israel, na viongozi wa pande mbili kutembeleana.

Licha ya kudai kuwa hakuna afisa yeyote wa ngazi ya juu wa Sudan aliyeitembelea Israel, lakini duru za habari siku chache zilizopita ziliarifu kuwa, kiongozi huyo wa kijeshi aliyeongoza mapinduzi nchini Sudan amefanya safari ya siri mjini Tel Aviv.

Haya yanajiri siku chache baada ya wananchi wa Sudan kufanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum, kulaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel na utawala wa majenerali wa kijeshi nchini mwao.

Wasudan katika maandamano ya kulaani kuanzishwa uhusiano na Israel

Katika maandamano hayo ya Alkhamisi iliyopita, waandamanaji walibeba mabango ambayo baadhi yake yalikuwa yameandikwa maneno yafuatayo: "Abdul Fattah al Burhan, kibaraka wa utawala wa Kizayuni; ataanguka tu."

Mwezi Oktoba 2021, wanajeshi wa Sudan walifanya mapinduzi mengine wakiongozwa na Jenerali al-Burhan na waliipindua serikali ya Waziri Mkuu Abdullah Hamdok, ambayo ilikuwa inashirikisha pia raia. 

 

Tags