Al-Burhan: Jeshi la Sudan litatimiza ahadi ya kuitisha uchaguzi 2023
Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan amesisitiza kuwa, jeshi litatimiza ahadi yake ya kuitisha uchaguzi katikati ya mwaka 2023 na wala halina nia ya kurefusha kipndi cha utawala mpito.
Sudan imetumbukia kwenye lindi la machafuko na mapigano kati ya jeshi na raia wanaopinga utawala wa kijeshi, tangu wanajeshi walipofanya mapinduzi Oktoba 25, 2021. Licha ya wanajeshi kuahidi kwamba watakabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia, lakini wananchi wanaopinga nchi hiyo kutawaliwa na jeshi wanataka majenerali wa jeshi wang'atuke madarakani na nchi hiyo kuongozwa katika kipindi cha mpito na utawala wa kiraia kuelekea uchaguzi wa kidemokrasia.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik, Abdel Fattah al-Burhan ametangaza kuwa, utakapofanyika uchaguzi nchini Sudan, jeshi litajiondoa kwenye ulingo wa siasa.
Hivi karibuni, Sudan imekuwa uwanja wa maandamano makubwa ya kupinga hatua zilizochukuliwa na Jenerali al-Burhan ikwemo kutangaza hali ya hatari na kulivunja Baraza la Utawala na Baraza la Mpito la Mawaziri. Wapinzani wanasema, hatua hizo ni aina fulani ya mapinduzi ya kijeshi.
Hata hivyo kiongozi huyo wa kijeshi amekanusha tuhuma hizo na kudai kuwa, lengo lake ni kurekebisha muelekeo wa kipindi cha mpito na kwamba atakabdhi madaraka ya nchi kwa serikali ya mpito.../