Shambulio la anga la Nigeria laua watoto saba, lajeruhi watano nchini Niger
(last modified Mon, 21 Feb 2022 07:44:14 GMT )
Feb 21, 2022 07:44 UTC
  • Shambulio la anga la Nigeria laua watoto saba, lajeruhi watano nchini Niger

Watoto saba wameuawa na wengine watano wamejeruhiwa katika shambulio la anga ambalo imeelezwa kuwa limefanywa kimakosa na jeshi la Nigeria katika eneo la Maradi kusini mwa Niger.

Kwa mujibu wa gavana wa eneo hilo Chaibou Aboubacar, shambulio hilo la anga lililofanywa katika eneo la mpakani mwa nchi mbili siku ya Ijumaa iliyopita lilikuwa limelenga wale waliotajwa kuwa ni maharamia wanaobeba silaha.

Aboubacar ameongeza kuwa, shambulio hilo lililolenga kijiji cha Nachade limesababisha maafa kwa watoto 12, ambapo saba wameuawa na watano wamejeruhiwa.

Kwa mujibu wa gavana huyo wa Maradi, watoto wanne waliuawa papo hapo na wengine watatu walifariki njiani kwa majeraha wakati walipokuwa wakiwahishwa hospitalini.

Amesema, wazazi wa watoto hao walikuwa wakihudhuria shughuli na yumkini watoto wenyewe walikuwa wanacheza walipolengwa na shambulio hilo la anga la jeshi la Nigeria.

Akina mama waliokuwa kwenye shughuli kwenye eneo la Niger lililoshambuliwa na ndege za kivita za jeshi la Nigeria

Chaibou Aboubacar ameendelea kueleza kwamba, anavyoamini, ndege za kijeshi za Nigeria zilikuwa zikiwalenga "maharamia wanaobeba silaha" katika maeneo ya mpakani lakini zilikosea shabaha na kukilenga kijiji cha Nachade.

Kadhalika, afisa huyo ameeleza kuwa aliyazuru makaburi ya watoto hao siku ya Jumamosi na eneo lililokumbwa na shambulio hilo.

Manispaa kadhaa za mkoa wa Maradi nchini Niger zinaathiriwa vibaya na machafuko ya magenge yaliyojizatiti kwa silaha nzito kutoka majimbo jirani ya Nigeria ya Katsina, Sokoto na Zamfara. 

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, mkoa wenyewe wa Maradi umewapa hifadhi wakimbizi wapatao elfu kumi kutoka Nigeria waliolazimika kuhama makazi yao kutokana na kuandamwa na mashambulio makali.../

Tags