Kwa akali watu 17 wauawa katika mapigano ya makundi hasimu Darfur, Sudan
Kwa akali watu 17 wameuawa huko Darfur magharibi mwa Sudan baada ya kuibuka mapigano baina ya makundi mawili hasimu.
Mauaji hayo yametokea siku chache baada ya kuripotiwa mauaji mengine kama hayo mwanzoni mwa juma hili. Adam Rigal, msemaji wa Kamati Kuu ya Wakimbizi wa Darfur amesema kuwa, vijiji vinne vimechomwa moto na kuteketezwa kikamilifu huku makumi ya watu wakijeruhiwa katika mapigano ya kikabila katika mkoa wa Darfur magharibi nchini Sudan.
Afisa huyo amewatuhumu wapiganaji wa kundi la Janjaweed kwamba ndio chanzo cha machafuko na mauaji katika eneo hilo.
Hitilafu za kugombania ardhi baina ya makabila ya Waarabu na wasio Waarabu katika eneo lenye milima mingi la Jebel Moon mkoa wa Darfur Magharibi zimesababisha mapigano ya umwagaji damu na mauaji ya mamia ya watu tokea Novemba mwaka jana hadi sasa.
Eneo la Darfur mwaka 2003 lilikumbwa na mapigano ya umwagaji damu kati ya serikali ya wakati huo ya Sudan chini ya uongozi wa Rais aliyeondolewa madarakani, Omar Hassan al-Bashir, na wapinzani wa serikali.
Malaki ya watu waliuawa na mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi katika mashambulizi hayo, na tokea wakati huo, eneo hilo limekuwa uwanja wa mapigano na umwagaji damu.
Ripoti mbalimbali za mashirika ya utoaji misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa zimekuwa zikitahadharisha kwamba, hali ya kibinadamuu katika eneo hilo ni mbaya sana.