Watu 100 wauawa katika shambulio la kigaidi kaskazini magharibi ya Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i81296-watu_100_wauawa_katika_shambulio_la_kigaidi_kaskazini_magharibi_ya_nigeria
Watu wapatao 100 wameuawa katika shambulio lililofanywa na kundi la maharamia na magaidi kaskazini magharibi mwa Nigeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 12, 2022 04:30 UTC
  • Watu 100 wauawa katika shambulio la kigaidi kaskazini magharibi ya Nigeria

Watu wapatao 100 wameuawa katika shambulio lililofanywa na kundi la maharamia na magaidi kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Shirika la habari la Iran Press limeripoti kuwa, watu wapatao 100 wakiwemo askari 19 wameuawa katika shambulio lililofanywa na kundi la maharamia na magaidi wenye silaha katika jimbo la Kebbi kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Adamu Zauro, kamanda wa vikosi vya valantia katika jimbo la Kebbi ambavyo vinafanya kazi ya kuwalinda raia na mashambulio ya maharamia wanaobeba silaha na magaidi amesema, waliokota maiti nyingi kwenye msitu wa jimbo hilo hapo jana.

Kwa mujibu wa Zauro, kazi ya kutafuta maiti zingine ingali inaendelea.

 

Shambulio hilo limejiri siku chache baada ya askari wengine wa kujitolea katika eneo la Sakaba jimboni humo kushambuliwa na maharamia na magaidi wakati walipokuwa katika doria.

Jeshi la Nigeria halijachukua hatua yoyote kuhusiana na shambulio hilo hadi sasa, lakini Nafiu Abubakar, afisa wa mawasiliano ya umma wa Polisi ya jimbo la Kebbi amethibistisha kuwa watu wasiopungua 100 wameuliwa katika shambulio la kigaidi lililotokea jimboni humo.

Kwa miaka kadhaa sasa maeneo ya kaskazini magharibi na katikati ya Nigeria yamekuwa yakishambuliwa kila mara na makundi yenye silaha, yanayovamia vijiji na kufanya jinai za mauaji na kuteka watu nyara ili kutolesha vikomboleo mbali na kupora mali za raia.

Hayo yanajiri huku serikali kuu ya Nigeria ikishindwa hadi sasa kurejesha nidhamu na usalama katika maeneo hayo.../