'Kafyu' yatangazwa kaskazini magharibi mwa Nigeria baada ya 83 kuuawa
Serikali ya jimbo la Kaduna la kaskazini magharibi mwa Nigeria imetoa agizo la kutotoka nje nyakati za usiku na mchana, baada ya makumi ya watu kuuawa katika mashambulizi ya makundi ya wabeba silaha katika eneo hilo.
Serikali ya jimbo hilo imetangaza 'kafyu' ya saa 24 katika miji ya Jema’a na Kaura, baada ya watu wasiopungua 83 kuuawa katika wimbi jipya la mashambulio ya magenge ya wabeba silaha katika maeneo ya kaskazini magharibi mwa nchi.
Inaarifiwa kuwa, watu 26 wameuawa katika miji ya Mararaban Agban, Agban na Adan katika eneo la Kaura, mbali na wengine wengi kujeruhiwa. Aidha nyumba zaidi ya 70 zimechomwa moto kwenye hujuma hiyo ya Machi 20.
Kabla ya hapo, watu 16 waliuawa katika shambulizi jingine la genge la wabeba silaha katika kijiji cha Ganar-Kiyawa, wilaya ya Bukkuyum jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa Nigeria.
Hata hivyo vyombo vya habari katika eneo hilo vimesema idadi ya wanakijiji waliouawa katika shambulio hilo jipya la magenge ya wabeba silaha jimboni Zamfara ni watu 37, akiwemo chifu wa kijiji hicho.
Aidha watu wengine wapatao 20 wameuawa katika kijiji cha Ganar-Kiyawa, eneo la Bukkuyum jimboni Zamfara katika shambulio jingine tofuti.
Maafisa usalama jimboni Kaduna wamewataka wakazi wa eneo hilo kuzingatia kafyu hiyo ya saa 24, ili vyombo vya usalama vifanye msako na operesheni ya kuwasaka wahalifu waliotekeleza mauaji hayo.