Watu 8 wauawa baada ya magaidi kushambulia treni Kaduna, Nigeria
Watu wasiopungua wanane wameuawa katika shambulizi la kigaidi lililolenga treni ya abiria jimboni Kaduna, kaskazini mwa Nigeria.
Hayo yalisemwa jana Jumanne na Samuel Aruwa, msemaji wa Idara ya Usalama wa Ndani katika Ofisi ya Kamishna wa jimbo la Kaduna na kuongeza kuwa, watu hao waliuawa na wengine 26 kujeruhiwa baada ya magaidi kushambulia treni iliyokuwa imebeba abiria 362 jimbo hapo.
Amesema wahudumu wa Shirika la Reli la Nigeria (NRC) na maafisa usalama si miongoni mwa watu waliouawa katika shambulizi hilo dhidi ya garimoshi lililokuwa likitokea Abuja, mji mkuu wa Nigeria.
Makamu wa Rais wa Nigeria, Yemi Osinbajo amewatembelea majeruhi wa hujuma hiyo hospitalini jimboni Kaduna, kaskazini magharibi mwa nchi.
Hili ni shambulizi la pili la kigaidi dhidi ya treni ya abiria katika eneo hilo la nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Hakuna kundi lililotangaza kuhusika nalo hadi tunamaliza kuandaa taarifa hii.
Nchi ya Nigeria imeendelea kushuhudia mauaji hasa katika maeneo ya kaskazini na mashariki mwa nchi hiyo kutokana na kuweko harakati za kundi la kigaidi la Boko Haram.