Watu 168 hawajulikani waliko baada ya magaidi kushambulia treni Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i82156-watu_168_hawajulikani_waliko_baada_ya_magaidi_kushambulia_treni_nigeria
Shirika la Reli la Nigeria (NRC) imetangaza kuwa hatima ya watu 168 haijulikani mpaka sasa, kufutia shambulizi la kigaidi lililolenga treni ya abiria jimboni Kaduna, Kaskazini mwa nchi siku chache zilizopita.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Apr 05, 2022 02:44 UTC
  • Watu 168 hawajulikani waliko baada ya magaidi kushambulia treni Nigeria

Shirika la Reli la Nigeria (NRC) imetangaza kuwa hatima ya watu 168 haijulikani mpaka sasa, kufutia shambulizi la kigaidi lililolenga treni ya abiria jimboni Kaduna, Kaskazini mwa nchi siku chache zilizopita.

Watu wasiopungua wanane waliuawa katika shambulizi hilo la kigaidi lililolenga treni ya abiria jimboni Kaduna, Kaskazini Magharibi mwa Nigeria usiku wa Machi 28.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli la Nigeria, Fidet Okhiria amesema abiria 168 waliokuwemo kwenye garimoshi hilo lililokuwa likitokea Abuja, mji mkuu wa Nigeria liliposhambuliwa, wametoweka.

Okhiria amesema simu za rununu za abiria 146 miongoni mwa waliotowekwa kufuatia hujuma hiyo, ama hazipokewi na wahusika, au zimezimwa. Amesema hawajui sababu za kutopokelewa simu za watu hao kila wanapopigiwa.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Shirika la Reli la Nigeria amesema abiria 186 wamewasili majumbani mwao salama salmini, huku abiria 22 tu wakiripotiwa kutoweka na familia zao.

Samuel Aruwa, Msemaji wa Idara ya Usalama wa Ndani katika Ofisi ya Kamishna wa jimbo la Kaduna alisema mbali na watu wanane kuuawa, wengine 26 walijeruhiwa baada ya magaidi kushambulia treni iliyokuwa imebeba abiria 362.

Hilo lilikuwa shambulizi la pili la kigaidi dhidi ya treni ya abiria katika eneo hilo la nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Hata hivyo hakuna kundi lililotangaza kuhusika na shambulizi hilo hadi sasa.  Nchi ya Nigeria imeendelea kushuhudia mauaji na mashambulizi ya kigaidi hasa katika maeneo ya kaskazini na mashariki mwa nchi hiyo kutokana na kuweko harakati za kundi la kigaidi la Boko Haram.