Mashirika ya haki za binadamu yakosoa mauaji ya kikabila Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i82206-mashirika_ya_haki_za_binadamu_yakosoa_mauaji_ya_kikabila_ethiopia
Makundi mawili ya kutetea haki za binadamu yamewatuhumu wanamgambo wanaobeba silaha wa kaskazini mwa Ethiopia kwa kutenda jinai za kivita.
(last modified 2024-06-01T06:57:28+00:00 )
Apr 06, 2022 06:09 UTC
  • Mashirika ya haki za binadamu yakosoa mauaji ya kikabila Ethiopia

Makundi mawili ya kutetea haki za binadamu yamewatuhumu wanamgambo wanaobeba silaha wa kaskazini mwa Ethiopia kwa kutenda jinai za kivita.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Novemba 4 mwaka juzi aliliamuru jeshi la nchi hiyo kuyashambulia maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo khususan eneo la Tigray baada ya kuwatuhumu wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) kuwa wamevishambulia vikosi vya jeshi la nchi hiyo. 

Shirika la Amnesty International na lile la Human Rights Watch (HRW) leo Jumatano yamewatuhumu wanamgambo wanaobeba silaha katika eneo la Amhara kaskazini mwa Ethiopia kuwa wanafanya kila wawezalo kutekeleza maangamizi ya kikabila vitani katika eneo la Tigray; ambapo hadi sasa maelfu ya raia wameuawa na wengine zaidi ya milioni moja wamekuwa wakimbizi. 

Wanamgambo wenye silaha wa eneo la Amhara Ethiopia 

Taarifa ya mashirika hayo mawili ya haki za binadamu imeeleza kuwa, hatua zinazotekelezwa na viongozi wa Amhara, wapiganaji maalumu wa kieneo na wanamgambo katika mapigano huko magharibi mwa Tigray ni sawa na kutenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu. Amnest International na HRW pia yamelituhumu jeshi la Ethiopia kuwa linahusika katika jinai hizo.  

Kenneth Roth Mkurugenzi Mtendaji wa Human Rights Watch amesema kuwa viongozi na askari usalama wa eneo la Amhara wametekeleza hatua za kikatili na unyama za maangamizi ya kizazi dhidi ya watu wa Tigray magharibi mwa eneo hilo.