Serikali ya Ethiopia yakanusha kuondoka wapiganaji wa Tigray huko Afar
Serikali ya Ethiopia imekanusha madai kwamba ilitangaza kuwa wapiganaji wa Tigray wameondoka katika mji wa Afar.
Msemaji wa serikali ya Ethiopia, Legesse Tulu ameeleza kuwa, taarifa zilizoenea kwamba wapiganaji wa Tigray wameondoka katika mji wa Afar ni za uwongo. Serikali imethibitisha kuwa wapiganaji hao waasi bado wapo huko Afar.
Ahmed Harif, Kamishna wa Polisi katika mji wa Afar ameeleza kuwa, wapiganaji wa Tigray bado wapo katika wilaya nne zinazoizunguka Tigray yaani Koneba, Abala, Barhale na Magale.
Huku haya yakiarifiwa, Getachew Reda Msemaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) amekataa kutoa maelezo kuhusu suala hilo. Jumatatu iliyopita Reda alieleza kuwa, wapiganaji wa kundi hilo la waasi wanaondoka Afar.
Wapiganaji wa Tigray kwa upande wao wamesema kuwa, wanaondoka Afar ili kuruhusu misafara ya misaada ya kibinadamu kuingia katika mji huo.
Tarehe 25 Machi mwaka huu serikali ya Ethiopia ilitangaza usitishaji vita wa upande mmoja ikisema kuwa utasaidia misaada ya kibinadamu kuelekea Tigray. Wapiganaji wa Tigray pia walikubali kuheshimu usitishaji vita huo kwa sharti kwamba misaada ya kutosha itumwe katika eneo hilo katika muda mwafaka.
Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umesema, hadi kufikia sasa malori 145 ya misaaada yamewasili Tigray tangu kutangazwa usitishaji vita kati ya pande mbili.