Guinea Conakry yaainisha muhula wa kipindi cha mpito cha miezi 36
Baraza la Taifa la Guinea la The Rally for Development (CNRD) limetangaza kipindi cha serikali ya mpito nchini humo kuelekea katika utawala wa kiraia kwa muda wa miaka mitatu au miezi 36.
Uamuzi huo uliochukuliwa jana Jumatano imeiweka Guinea Conakry katika hali ya msuguano na washirika wa kikanda na Umoja wa Mataifa; ambao wametoa wito wakitaka muhula mfupi zaidi wa serikali ya mpito nchini. Pamoja na kuainisha muhula huo wa kipindi cha mpito, lakini wanajeshi walioko madarakani wameahidi kuirejesha nchi katika utawala wa kiraia.
Mkuu wa utawala wa kijeshi nchini Guinea, Kanali Mamadou Doumbouya alimpindua madarakani Rais Alpha Conde mwezi Septemba mwaka jana na tangu wakati huo amejitangaza kuwa kiongozi wa Guinea Conakry.
Guinea Conakry pia kama ilivyokuwa huko Mali na Burkina Faso, nchi mbili nyingine za Magharibi mwa Afrika ambako majeshi yametwaa madaraka imesimamishwa kwa muda uanachama wake katika Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS).
Ecowas ilitoa wito wa kurejeshwa haraka utawala wa kiraia huko Guinea baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomuengua Rais wa nchi hiyo Alpha Conde.
Hii si mara ya kwanza kwa kiongozi wa kijeshi wa Guinea Conakry kutangaza kipindi cha mpito; kwani mapema mwezi huu alitangaza kipindi cha miezi 39 ya utawala wa mpito kabla ya taifa hilo la Afrika magharibi kurejea kwenye utawala wa kiraia. Kanali Mamadou Doumbouy alichukua hatua hiyo baada ya uongozi wa kijeshi wa nchi hiyo kukosolewa pakubwa kieneo na kimataifa kuhusu suala hilo.