Kenya na Uturuki zakubaliana kushirikiana katika kubadilishana taarifa za usalama
Marais wa Kenya na Uturuki wamekubaliana nchi zao mbili kushirikiana katika kubadilishana taarifa za usalama na za kiintelijinsia kwa lengo la kuzima uwezekano wa kutokea mashambulio ya kigaidi.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki wameyaelezea makubaliano hayo waliyofikia mjini Nairobi kuwa ni hatua chanya katika kudhamini usalama wa nchi hizo mbili.
Ripoti kutoka nchini Kenya zinaeleza kuwa kushirikiana kwa karibu zaidi Nairobi na Ankara katika kurejesha uthabiti nchini Somalia ni suala jengine lililoafikiwa baina ya Kenyatta na Erdoğan katika mazungumzo yao hayo.
Baada ya mazungumzo yake na mwenzake wa Kenya, Rais wa Uturuki amesema Kenya inakabiliwa na vitisho vya usalama vinavyotokana na ugaidi na misimamo ya kufurutu mpaka, hususan vinavyotokea nchi jirani ya Somalia na kwamba Uturuki inaiunga mkono Kenya katika kukabiliana na vitisho hivyo.
Baada ya kuhatimisha safari yake nchini Uganda, Rais wa Uturuki, Jumatano usiku aliwasili mji mkuu wa Kenya , Nairobi kuendelea na awamu ya pili ya safari yake.../