EALA yandaa muswada wa sheria ya kukabili ukeketaji
(last modified Sat, 04 Jun 2016 07:40:19 GMT )
Jun 04, 2016 07:40 UTC
  • EALA yandaa muswada wa sheria ya kukabili ukeketaji

Bunge la Afrika Mashariki EALA linaandaa muswada ambao ukipasishwa na kuwa sheria, utamaduni wa kuwakeketa mabinti na wanawake utapigwa marufuku katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC.

EALA imemruhusu Dora Byamukama, mbunge wa bunge hilo la kieneo kutoka Uganda kutoshiriki vikao na badala yake aandae Muswada wa Sheria ya Kupiga Marufuku Ukeketaji wa Mwaka 2016.

Mbunge huyo amesema baada ya kuidhinishwa protokali ya soko la pamoja miongoni mwa nchi wanachama wa EAC, kuna hatari ya kuenea kwa kasi utamaduni wa ukeketaji miongoni mwa jamii tofauti za kanda ya Afrika Mashariki. Akiashiria baadhi ya taathira hasi za ukeketaji, mbunge huyo wa Bunge la Afrika Mashariki amesema mila hiyo imesababisha mabinti wengi kukatiziwa masomo na kusukumwa katika ndoa za mapema, kupata matatizo wakati wa kujifungua na wakati wa hedhi, kuambukizwa virusi vya HIV/UKIMWI, kuvuja damu kupita kiasi na hatimaye kuaga dunia. Akichangia hoja ya kuandaliwa muswada huo, mbunge wa EALA kutoka Kenya Judith Pareno amesema kuna haja ya kukabiliwa ukeketaji huku akibainisha takwimu za Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF zinazosema kuwa, wanawake milioni 200 kutoka nchi 27 za bara Afrika wamekeketwa mwaka huu pekee. Nchi zinazosemekana kuongoza kwa tatizo hilo barani Afrika ni Djibouti, Misri, Eritrea, Guinea, Mali, Sierra Leone, Somalia na Sudan. Kadhalika mbali na Indonesia, Iraqi Kurdistan na Yemen, utamaduni wa kuwakeketa mabinti umesambaa katika baadhi ya nchi za bara Asia na Mashariki ya Kati.

Tags