Jun 08, 2022 10:47 UTC
  • ECOWAS yaikosoa Mali kwa kurefusha kipindi cha mpito

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) imeeleza kusikitishwa kwake na hatua ya Mali ya kurefusha kipindi cha mpito kwa miezi 24.

ECOWAS imesema ni jambo la kusikitisha kwa utawala wa muda wa Mali kurefusha muda wake wa kuwa uongozini katika hali ambayo, pande mbili hizo zinaendelea kufanya mazungumzo ya kujaribu kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa na kiuongozi unaolikabili taifa hilo la Afrika Magharibi.

Juzi Jumatatu, utawala wa kijeshi ambao ulitwaa madaraka kwa mara ya kwanza mnamo Agosti mwaka 2020, ulitoa dikrii inayosema kuwa, kipindi cha mpito cha miezi 24 kinaanza kuhesabiwa kuanzia Machi mwaka huu 2022.

Hivi karibuni, viongozi wa ECOWAS waliokutana Accra, mji mkuu wa Ghana walishindwa kuafikiana kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya tawala za kijeshi katika mataifa ya Mali, Burkina Faso na Guinea.

Watawala wa kijeshi Mali

Jumuiya hiyo ya kieneo yenye nchi wanachama 15 imekuwa ikiwashinikiza watawala wa kijeshi Mali wasirefushe kipindi cha mpito kwa zaidi ya miezi 16.

Januari mwaka huu, ECOWAS iliwawekea vikwazo vikali watawala hao wa kijeshi wa Mali, baada ya kutangaza kuwa hawatoandaa uchaguzi wa kidemokrasia mwezi uliofuata, kama ilivyokuwa imeratibiwa. 

Tags