Ethiopia yabuni kamati ya kuzungumza na wapiganaji wa Tigray
Waziri Mkuu wa Ethiopia amesema serikali ya federali ya nchi hiyo imeunda kamati ya kufanya mazungumzo na vikosi vya Harakati ya Ukombizi wa Watu wa Tigray (TPLF).
Abiy Ahmed alisema hayo jana Jumanne akilihutubia Bunge la nchi hiyo na kufafanua kuwa: Kuhusu amani, kuna kamati imebuniwa. Mazungumzo yanahitaji kazi kubwa. Kamati hiyo iliyoundwa itathmini namna tutakavyofanya mazunugumzo yenyewe.
Tarehe 25 Machi mwaka huu, serikali ya Ethiopia ilitangaza usitishaji vita wa upande mmoja ikisema kuwa utasaidia misaada ya kibinadamu kuelekea Tigray.
Wapiganaji wa Tigray pia walikubali kuheshimu usitishaji vita huo kwa sharti kwamba misaada ya kutosha itumwe katika eneo hilo katika muda mwafaka.
Tangu mwezi Novemba mwaka juzi eneo la Tigray limekumbwa na hitilafu na mivutano ya kisiasa kati ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed na viongozi wa eneo hilo ambao wakati fulani waliongoza serikali ya Ethiopia.
Vita vilivyoshuhudiwa katika eneo hilo hadi sasa vimesababisha kuuliwa makumi ya maelfu ya watu na kupelekea mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.