Abiy Ahmed: Waasi wa OLA wameua raia wengine kwa umati Oromia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i85526-abiy_ahmed_waasi_wa_ola_wameua_raia_wengine_kwa_umati_oromia
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed amelituhumu kundi la waasi linalojiita Jeshi la Ukombozi wa Oromo (OLA) kuwa limefanya mauaji mapya ya halaiki katika eneo la Oromia, magharibi mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 06, 2022 01:48 UTC
  • Abiy Ahmed: Waasi wa OLA wameua raia wengine kwa umati Oromia

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed amelituhumu kundi la waasi linalojiita Jeshi la Ukombozi wa Oromo (OLA) kuwa limefanya mauaji mapya ya halaiki katika eneo la Oromia, magharibi mwa nchi.

Abiy Ahmed amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kufafanua kuwa: Wakazi wa zoni ya Qellem Wollega jimboni Oromia wameuawa kwa umati. Tutalifuatilia kundi hilo la kigaidi mpaka mwisho na kulisambaratisha.

Hata hivyo Ofisi ya Waziri Mkuu huyo wa Ethiopia haijaeleza idadi ya raia, waasi wa OLA au maafisa usalama wa nchi hiyo waliouawa au kujeruhiwa katika mapigano hayo mapya katika eneo la Oromia. 

Vyombo vya habari katika eneo hilo vimetangaza kuwa, vimehesabu maiti zaidi ya 300 katika shambulio hilo la Jumatatu la waasi lililolenga watu wa jamii ya Amhara, katika kijiji kimoja kilichoko katika wilaya ya Hawa Gelan, eneo la Qellem Wollega.

Mwezi uliopita, watu kati ya 260 na 320, wengi wao kutoka kabila la Amhara, waliuawa katika shambulio jingine lililofanyika katika eneo la Oromia ambalo akthari ya wakazi wake ni watu wa jamii ya Oromo. Addis Ababa iliwanyooshe tena kidole cha lawama wapiganaji wa Jeshi la Ukombozi wa Oromo (OLA).

Haya yanaripotiwa katika hali ambayo, serikali ya Ethiopia inajiandaaa kufanya mazungumzo ya amani na waasi wa Tigray yanayotazamiwa kufanyika Nairobi, mji mkuu wa Kenya; katika jitihada za kumaliza mgogoro wa umwagaji damu uliodumu kwa miezi 18 kaskazini mwa nchi hiyo.