Watu kadhaa wauawa katika shambulio la anga Tigray, Ethiopia
Watoto watatu ni miongoni mwa watu saba waliouawa katika shambulio la anga lililolenga uwanja wa kucheza watoto katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.
Duru za hospitali katika mji wa Mekelle eneo la Tigray zimesema watu kadhaa wamejeruhiwa pia katika shambulio hilo la jana Ijumaa. Hata hivyo serikali ya federali ya Ethiopia kupitia msemaji wake, Legesse Tulu imekanusha madai ya kutokea vifo katika hujuma hiyo ya anga.
Huku hayo yakijiri, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitaka pande husika katika mgogoro huo kutoa kipaumbele kwa diplomasia na mazungumzo na kutoshadidisha mgogoro huo wa Tigray.
Kabla ya hapo, Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika alisema ametiwa wasiwasi na ripoti za kuibuka makabiliano mapya ya kijeshi nchini Ethiopia.
Amezitaka pande hasimu katika mgogoro wa eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia kujizuia na hatua zitakazoshadidisha hali ya mambo, na watafute ufumbuzi kwa njia za amani.
Aidha Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Mashariki mwa Afrika na pembe ya Afrika IGAD imezitaka pande husika kujiepusha mara moja na hatua za kiuhasama zinazoweza kupelekea hali ya mambo kuwa mbaya zaidi.
Vita vilivyoshuhudiwa katika eneo hilo kati ya askari wa serikali na wapiganaji wa TPLF tokeo Novemb 2020 vimesababisha kuuliwa makumi ya maelfu ya watu na kupelekea mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi.