Mkuu wa UNHCR awataka wahisani waisaidie Tanzania kwa inavyoendelea kukirimu wakimbizi
Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR amewahimiza wahisani kuunga mkono zaidi suluhu na hiari juu ya suala la wakimbizi na kusifu maendeleo yaliyopigwa katika ulinzi wa wakimbizi nchini Tanzania.
Filippo Grandi, ameyasema hayo jana wakati akihitimisha ziara yake nchini humo na kubainisha kuwa miongoni mwa suluhu hizo ni pamoja na hatua endelevu ya wakimbizi kurudi nyumbani kwa hiari.
Katika ziara yake ya siku tatu, Grandi amekutana na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na kujadili umuhimu wa kuweka mazingira mazuri ya kurejea nyumbani wakimbizi wa Burundi, huku akihakikisha wakimbizi wote nchini Tanzania wanalindwa na kusaidiwa.
Kwa sasa Tanzania inahifadhi zaidi ya wakimbizi na watafuta hifadhi 248,000, hasa wanaotoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na wengi wao wanaishi katika kambi za wakimbizi za Nduta na Nyarugusu katika mkoa wa Kigoma kaskazini mashariki ya nchi hiyo.
Tangu Septemba 2017, takriban wakimbizi 142,000 wa Burundi wamerejea nchini kwao kwa hiari.
 
Grandi ameipongeza Tanzania na wananchi wake kwa historia yao ya muda mrefu ya kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi, pamoja na juhudi za kuendeleza ulinzi na suluhisho kwa wakimbizi nchini humo, kwa kuzingatia mkataba wa kimataifa wa wakimbizi.
"Kwa kweli nimetiwa moyo na juhudi za serikali za kuimarisha ulinzi wa wakimbizi, na kusimama pamoja nao. Ahadi ya UNHCR ya kuunga mkono Tanzania na kulinda haki za wakimbizi wanaohifadhiwa hapa bado ni thabiti", amesisitiza Grandi.
Mkuu huyo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, amepongeza pia juhudi za hivi karibuni za serikali ya Tanzania za kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wakimbizi, akibainisha kuwa hatua hiyo itawapa ulinzi muhimu wa kisheria na kupunguza hatari ya kutokuwa na utaifa, huku pia ikitoa aina ya utambulisho wanaporejea katika nchi yao ya asili.
Kufikia Agosti 2022, UNHCR ilikuwa imepokea asilimia 27 pekee ya fedha zinazohitajika nchini Tanzania kwa mwaka huu.../
 
							 
						 
						