Watoto 22,500 waaga dunia kwa kuvuta hewa chafu Lagos, Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i87622-watoto_22_500_waaga_dunia_kwa_kuvuta_hewa_chafu_lagos_nigeria
Watoto zaidi ya 22,500 walipoteza maisha mwaka jana 2021 katika jimbo lenye idadi kubwa zaidi ya watu la Lagos, kusini magharibi mwa Nigeria kutokana na kuvuta hewa.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Aug 30, 2022 21:51 UTC
  • Watoto 22,500 waaga dunia kwa kuvuta hewa chafu Lagos, Nigeria

Watoto zaidi ya 22,500 walipoteza maisha mwaka jana 2021 katika jimbo lenye idadi kubwa zaidi ya watu la Lagos, kusini magharibi mwa Nigeria kutokana na kuvuta hewa.

Takwimu hizo mpya zimetolewa na Dolapo Fasawe, Mkuu wa Shirika la Kulinda Mazingira la Jimbo la Lagos (LASEPA) na kueleza kuwa, serikali inafanya jitihada za kuhakikisha kuwa wakazi wa jimbo hilo na nchi nzima kwa ujumla wanavuta hewa safi na kuishi katika mazingira salama.

Amesema jiji la Lagos lenye watu zaidi ya milioni 15, linafahamika kama kitovu cha fedha cha Nigeria, lakini uchafuzi wa hali ya hewa unasababisha magonjgwa na vifo vingi ambavyo vingeliweza kuepukika.

Takwimu za shirika la Global Burden of Disease zinaonesha kuwa, asilimia 78 ya vifo vinavyotokana na hali chafu ya hewa nchini Nigeria ni miongoni mwa watoto.

Hali chafu ya hewa

Kwa mujibu wa Maria Neira, Mkurugenzi wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira wa Shirika la Afya Duniani (WHO), asilimia 99 ya watu duniani wanaishi kwenye maeneo yenye kiwango cha juu zaidi cha uchafuzi wa hewa kuliko kilichowekwa na shirika hilo, uchafuzi unaosababisha mamilioni ya vifo kila mwaka.

Takwimu zinaonesha kuwa, uchafuzi wa hewa husababisha vifo vya watu milioni 1.1 barani Afrika kila mwaka, na hivyo kuwa chanzo kikuu cha pili cha vifo barani humo.