Umoja wa Mataifa: Hakuna suluhisho la kijeshi la mzozo wa Libya
Msaidizi wa Katibu Mkuu na Mratibu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amesisitiza kuwa, hakuna suluhisho la kijeshi kwa mzozo wa nchi hiyo, na kwa mara nyingine ametoa wito wa kufanyika uchaguzi nchini Libya haraka iwezekanavyo.
Raisedon Zenenga amesema, kipaumbele cha shirika hilo la kimataifa ni kushirikiana na pande zote nchini Libya ili kuwezesha mchakato wa kufikia mwafaka kuhusu kufanyika uchaguzi nchini Libya haraka iwezekanavyo.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, wananchi wa Libya wanataka kuchagua viongozi wao na kuanza kazi taasisi za nchi hiyo kupitia uchaguzi wa kidemokrasia.
Mgogoro wa kisiasa wa Libya umeongezeka katika siku za karibuni kati ya serikali ya umoja wa kitaifa inayoongozwa na Abdul Hamid Dbeibeh na serikali iliyopewa mamlaka inayoongozwa na Fathi Bashagha.
Mji wa Tripoli, mji mkuu wa Libya, hivi karibuni ulishuhudia kutumwa kwa vikosi vya kijeshi kutokana na uwezekano wa kutokea mapigano ya silaha kwa sababu ya tofauti za kisiasa kati ya serikali za Abdul Hamid Dbeibeh, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Fathi Bashagha, Waziri Mkuu mpya aliyeteuliwa na Bunge la nchi hiyo.

Hitilafu hizo zilizoambatana na kutumwa kwa vikosi vya jeshi mjini Tripoli, zimesababisha wasiwasi mkubwa.
Tangu kupinduliwa kwa aliyekuwa dikteta wa Libya, Muammar Gaddafi, mwaka 2011, nchi hiyo inaongozwa na serikali mbili tofautii za mashariki na magharibi mwa nchi hiyo.