Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya: Utulivu umerejea Tripoli
Serikali ya Umoja wa Kitaifa yenye makao yake makuu mjini Tripoli (GNU) ilisema jana Jumanne kuwa "imehitimisha" operesheni ya kijeshi katika mji mkuu huo, kufuatia usiku wa mapigano yaliyosababishwa na kuripotiwa mauaji ya kamanda mkuu wa usalama.
Wizara ya Ulinzi ya Libya chini ya serikali hiyo bila kutoa maelezo ya kina imesema katika taarifa yake kwamba, imetoa maagizo "kukamilisha mpango wake katika kanda ili kuhakikisha usalama na utulivu endelevu."
Mapigano yaliripotiwa kuzuka katika maeneo kadhaa ya Tripoli Jumatatu jioni baada ya mauaji ya Abdulghani al-Kikli, anayejulikana pia kama Ghaniwa, mkuu wa wanagambo wa Stability Support Authority (SSA).
Inasemekana alipigwa risasi ndani ya makao makuu ya Brigedi ya 444 kusini mwa jiji, kufuatia kile ambacho vyombo vya habari vya ndani vilielezea kama mazungumzo yaliyofeli.
Kwa mujibu wa Al Jazeera, milio ya risasi na milipuko ilisikika katika vitongoji vya Abu Salim na Mashrou mjini humo. Walioshuhudia walisema kuwa vikosi vya jeshi kutoka brigedi ya 111 na 444 vilivamia makao makuu ya SSA.
Picha zinazosambaa mtandaoni zilionekana kuonyesha majeruhi wengi, ingawa idadi kamili cha majeruhi na vifo hakijabainika. Al Jazeera iliripoti kuwa takriban watu sita walijeruhiwa.
Baadhi ya duru za habari zimesema watu sita waliuawa katika machafuko hayo ya Tripoli, baada ya watu wenye silaha kufyatuliana risasi ovyo katika wilaya za kusini mwa mji huo kufuatia mauaji ya Ghaniwa, kiongozi aliyekuwa na nguvu wa kundi la wanamgambo la SSA.