Trump apanga kuwahamishia Libya Wapalestina milioni 1 wa Gaza
Imefichuka kuwa, maafisa wakuu wa serikali ya Rais wa Marekani, Donald Trump wanashughulikia mpango wa kuhamisha takriban nusu ya wakazi milioni 2.2 wa Ukanda wa Gaza uliozingirwa na kuwapeleka hadi Libya.
Shirika la habari la NBC News limeripoti hayo na kueleza kuwa, mpango huo unakusudia kuhamishiwa katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini, Wapalestina zaidi ya milioni moja.
Watu wawili kati ya watano wenye ufahamu na mpango huo wamenukuliwa na NBC News wakisema kuwa, pendekezo hilo limepiga hatua kiasi kwamba limejadiliwa moja kwa moja na uongozi wa Libya.
Marekani imejitolea kuachia mabilioni ya dola za fedha za Libya zilizozuiwa, ikiwa nchi hiyo itakubali kuwapa makazi Wapalestina waliofurushwa kwenye makazi yao, vimesema vyanzo vitatu vya habari.
Duru hizo za habari zimearifu kuwa, utawala wa Israel umefahamishwa juu ya mazungumzo hayo, na kusisitiza kuwa hakuna makubaliano ya mwisho ambayo yamefikiwa kufikia sasa. Trump alikariri Alkhamisi kwamba, Marekani inapaswa "kuimiliki" Gaza na eti kuigeuza kuwa "eneo huru."
Hii ni katika hali ambayo, mwezi Machi mwaka huu, serikali ya Somali ilipinga vikali pendekezo la Marekani la kuwapa makazi Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza kwenye ardhi ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, Ahmed Moallim Fiqi alinukuliwa akisema, Somali haitaafiki pendekezo lolote linalokiuka haki ya Wapalestina kuishi kwa amani katika nchi yao.
Kabla ya hapo pia, maafisa wa serikali ya Sudan walipinga pendekezo hilo la Marekani, huku maafisa kutoka eneo lenye mamlaka ya ndani la Somaliland wakikana kuwepo mawasiliano ya aina yoyote kuhusiana na suala hili.