Wanamgambo 27 wa al Shabab wauawa katika shambulio la anga Somalia
wanamgambo 27 kundi la kigaidi la al Shabab la nchini Somalia wameuawa katika shambulio la anga lililotekelezwa katika mkoa wa kati wa Hiran ambako jeshi la Somalia na majeshi waitifaki yalianzisha oparesheni dhidi ya kundi hilo mwezi uliopita.
Itakumbukwa kuwa Marekani pia imekuwa ikitekeleza mashambulizi ya anga huko Somalia dhidi ya wanamgambo wa al Shabab wenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida kwa miaka kadhaa sasa.
Huko mkoani Hiran wakazi wa eneo hilo wanasema kuwa wanamgambo wa al Shabab wamekuwa wakichoma nyumba zao, wakivunja visima vya maji na kuuwa raia mambo yaliyowasukuma wenyeji wa mkoa huo kuendesha mapambano dhidi ya kundi kwa kushirikiana na serikali kuu ya Mogadishu.
Wanagambo hao wa al Shabab ambao wanasema lengo lao ni kuipindua serikali kuu ya Mogadishu inayoungwa mkono na nchi za Magharibi waliuliwa wakati wakitekeleza hujuma dhidi ya askari jeshi wa serikali karibu na Buulobarde, mji unaopatikana umbali wa kilomita 200 kaskazini mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Kamandi ya Marekani na Afrika (AFRICOM) imeripoti kuwa, mashambulizi hayo ya kujihami yameliwezesha jeshi la taifa la Somalia na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini humo (ATMIS) kuchukua hatua na kuendeleza oparesheni za kuwasambaratisha wanamgambo hao huko Hiraan katikati mwa Somalia.
Kwa upande wao wanaharakati wa haki za binadamu wamekuwa wakiilaumu Marekani kwa kuendesha oparesheni za siri huko Somalia na hivyo kutatiza suala la kutambuliwa idadi kamili ya raia wanaouawa katika hujuma na mashambulizi nchini humo.