Jeshi la Somalia laangamiza makamanda kadhaa wa al-Shabaab
Makamanda watatu waandamizi wa kundi la kigaidi la al-Shabab walioendesha wimbi la mashambulizi mabaya nchini Somalia katika miezi ya karibuni wameuawa katika operesheni ya pamoja ya usalama.
Wizara ya Habari, Utamaduni na Utalii ya Somalia imesema waliouawa ni pamoja na Nuur Abdi Rooble, ambaye alikuwa miongoni mwa magaidi makatili waliohusika na mashambulizi dhidi ya raia kote Somalia.
Alifariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa operesheni ya anga iliyoendeshwa na jeshi la Somalia na washirika wake wa usalama wa kimataifa, kwenye viunga vya mji wa El-Bur katikati mwa Somalia.
Rooble alijiunga na al-Shabab mwaka wa 2009, na kifo chake kimeleta pigo kubwa kwa mitandao ya kigaidi inayotishia maisha ya Wasomali, wizara imesema.
Makamanda wengine wakuu waliouawa wakati wa operesheni hiyo walitambuliwa kama Caddaw, aliyeuawa katika eneo la Galgaduud, na Macallin Cumar, kamanda aliyekuwa anahusika na mafunzo ya wanamgambo wa al-Shabab.
"Hii inaleta jumla ya idadi ya vinara wa al-Shabab walioangamizwa katika operesheni hiyo kufikia watano. Magaidi wote waliouawa walihusika katika kupanga na kutekeleza hujuma za kigaidi huko Hiiraan na Shabelle ya Kati," wizara imesema.