Watu 50 wauawa katika shambulio la anga dhidi ya shule nchini Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i88952-watu_50_wauawa_katika_shambulio_la_anga_dhidi_ya_shule_nchini_ethiopia
Watu wasiopungua 50 wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika shambulio la anga lililolenga shule moja huko kaskazini mwa Ethiopia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 06, 2022 04:13 UTC
  • Watu 50 wauawa katika shambulio la anga dhidi ya shule nchini Ethiopia

Watu wasiopungua 50 wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika shambulio la anga lililolenga shule moja huko kaskazini mwa Ethiopia.

Hayo yaliripotiwa jana Jumatano na shirika la habari la Reuters ambalo limeeleza kuwa, watu 70 wamejeruhiwa katika hujuma hiyo, katika eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia, karibu na mpaka wa Eritrea.

Wapiganaji wa Tigray wameiambia Reuters kuwa, shule hiyo ilikuwa inatumika kama sehemu ya muda ya kuwahifadhi wakimbizi walioathiriwa na vita vya ndani katika eneo hilo.

Baadhi ya duru za habari zinasema kuwa, waliouawa katika shambulio hilo la juzi Jumanne ni watu 65, mbali na makumi kujeruhiwa.

Hilo ni shambulizi la pili ndani ya wiki moja kushuhudiwa katika mji wa Adi Daero katika eneo la Tigray, ambapo watu 5 waliuawa huku wengine 16 wakijeruhiwa katika hujuma ya Septemba 30.

Mwishoni mwa Agosti pia, watoto watatu walikuwa miongoni mwa watu saba waliouawa katika shambulio jingine la anga lililolenga uwanja wa kucheza watoto katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.

Machafuko Tigray

Wimbi hilo la mashambulizi ya anga yanajiri katika hali ambayo, serikali ya Ethiopia kwa mara nyingine tena imesema imeafiki mwito wa Umoja wa Afrika (AU) wa kufanya mazungumzo ya amani bila masharti yoyote na waasi wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF).

Vita vilivyoshuhudiwa katika eneo hilo kati ya askari wa serikali na wapiganaji wa TPLF tokeo Novemba 2020 vimesababisha kuuliwa makumi ya maelfu ya watu na kupelekea mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi.