Guterres: Hali ya mambo Ethiopia huenda isidhibitike tena
(last modified Tue, 18 Oct 2022 07:35:31 GMT )
Oct 18, 2022 07:35 UTC
  • Guterres: Hali ya mambo Ethiopia huenda isidhibitike tena

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusu hali ya mambo nchini Ethiopia na kutoa mwito kwa pande hasimu katika mgogoro wa eneo la Tigray la kaskazini mwa nchi kuhitimisha mvutano na uhasama baina yao.

Antonio Guterres ametoa mwito huo katika kikao na waandishi wa habari Jumatatu ambapo ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu kushadidi kwa ghasia na athari zake kwa raia huko kaskazini mwa Ethiopia.

Guterres amebainisha kuwa: Mashambulizi ya kiholela, yakiwemo dhidi ya makazi ya raia, yanayua idadi kubwa ya watu wasio na hatia kila siku, kuharibu miundomsingi na kuzuia upatikanaji wa huduma muhimu.

Aidha Katibu Mkuu wa UN amelitaka jeshi la Eritrea kuondoka askari wake mara moja katika eneo la Tigray na kusisitiza kuwa, raia ndio wanaolipa 'gharama kubwa' ya mapigano na uhasama ulioibuka upya Agosti mwaka huu. 

Haya yanaripotiwa siku chache baada ya mazungumzo ya amani baina ya waasi wa TPLF na serikali ya Ethiopia ambayo yanasimamiwa na Umoja wa Afrika kuakhirishwa kwa sababu za kilojistiki.

Mgogoro wa eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia

Katika ripoti yake ya hivi karibuni, Tume ya Wataalamu wa Haki za Kibinadamu wa UN nchini Ethiopia iliangazia kile ilichokiita taarifa za kuaminika za mauaji makubwa yaliyofanywa na jeshi la ulinzi la taifa la Ethiopia, ambayo yaliwalenga wanaume na wavulana wa Tigray walio katika umri wa kupigana.

Ripoti hiyo ilisema ukiukaji wa haki za binadamu umefanywa na pande zote. Hata hivyo serikali ya Ethiopia iliiponda na kuikosoa vikali ripoti hiyo ya tume ya Umoja wa Mataifa na kueleza kwamba, imetawaliwa na matashi ya kisiasa na haina ukweli wowote ule ndani yake.