Oct 18, 2022 07:46 UTC
  • Askari walinda amani 3 wa UN wauawa nchini Mali

Askari watatu walinda amani wa Umoja wa Mataifa wameuawa baada ya msafara wao wa magari kukanyaga bomu huko kaskazini mwa Mali.

Duru za kiusalama na maafisa wa serikali ya Mali wametangaza kuwa, askari waliouawa ni raia wa Chad, na walikuwa wakifanya kazi chini ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali kinachojulikana kama MINUSMA. 

Mripuko huo wa bomu ulitokea jana Jumatatu yapata kilomita 10 kutoka mji wa Tessalit katika eneo la Kidal, kaskazini mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Mauaji hayo yamefanyika siku moja kabla ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufanya mkutano kuhusu ujumbe wake wa kulinda amani ulioko Mali.

Shambulizi la uwagaji mkubwa zaidi wa damu wa karibuni ni lile lililotokea Agosti mwaka huu katika mji wa Gao wa kaskazini mwa Mali ambalo liliua wanajeshi 42 wa nchi hiyo.

Kikosi cha amani cha UN nchini Mali

Genge la ukufurishaji liitwalo JNIM na ambalo lina mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida lilitangaza kuhusika na mashambulizi na mauaji hayo.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha luwa, askari walinda amani 28 wa umoja huo waliuawa na wengine 165 walijeruhiwa nchini Mali mwaka uliopita wa 2021.

Tags