Uturuki na Libya zasaini mikataba miwili ya ushirikiano wa kijeshi
Oct 26, 2022 12:57 UTC
Maafisa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya na wa Uturuki wametia saini mikataba miwili ya ushirikiano wa kijeshi mjini Istanbul.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr, ofisi ya Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya Abdulhamid Debibeh, imetangaza kuwa Debibeh mwenyewe na Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Hulusi Akar wametia saini mikataba miwili ya ushirikiano wa kijeshi kati ya Ankara na Tripoli.
Imeelezwa katika taarifa hiyo kwamba: mkataba wa pili unajumuisha utaratibu wa utekelezaji wa mkataba wa usalama uliosainiwa na Baraza la Urais la Serikali ya Makubaliano ya Kitaifa ya Libya mwaka 2019.
Katika mkataba wa kwanza, imesisitizwa kuhusu "utumiaji uzoefu wa Uturuki katika kuboresha ufanisi wa uwezo wa Jeshi la Anga la Jeshi la Libya".
Hafla ya utiaji saini mikataba hiyo miwili ilifanyika mjini Istanbul, Uturuki.

Mwishoni mwa Novemba 2019, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan na Fayez Siraj, aliyekuwa Rais wa Serikali ya Makubaliano ya Kitaifa ya Libya, ambayo inadhibiti sehemu tu ya ardhi ya Libya, walitia saini makubaliano yanayohusu maeneo ya baharini na ushirikiano wa kijeshi.
Mwaka 2011, nchi wanachama wa shirika la kijeshi la NATO zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya Libya kwa kisingizio cha kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi. Baada ya kupinduliwa Gaddafi, Libya iliingia katika kipindi cha machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vingali vinaendelea na hadi sasa nchi hiyo haijaweza kushuhudia amani na uthabiti.../
Tags