Haftar atishia kuanzisha vita vya kuikomboa Libya
Kamanda wa linalojiita jeshi la taifa la Libya ametishia kuwa, iwapo juhudi za sasa za kupata suluhisho la amani la mgogoro wa Libya zitafeli, ataanzisha vita vikubwa vya kuikomboa nchi hiyo.
Mgogoro wa kisiasa nchini Libya umeongezeka kati ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) inayoongozwa na "Abdul Hamid al-Dbeibeh", serikali iliyopewa mamlaka na Bunge inayoongozwa na "Fathi Bashagha", na vikosi vya jeshi huko Tripoli, mji mkuu wa nchi hiyo.
Jenerali mstaafu Khalifa Haftar amesema: "Baada ya michakato yote ya hapo kabla kufeli na kuwa na matokeo ya kukatisha tamaa, sasa tutaenda sambamba na nia na hamu ya watu wa Libya."
Haftar amesema kuwa: Kwa sasa tunakaribia kuchukua uamuzi muhimu utakaoambatana na irada na azma ya wananchi wa kukomboa nchi. Ameongeza kuwa, uzoefu na tajiriba vimethibitisha kuwa suluhisho au mpango wowote wa amani hautafanikiwa ila kwa kuungwa mkono na watu wa Libya. Ameongeza kuwa hali ya sasa ya Libya ni tofauti na hapo awali na harakati za wananchi za kuleta mabadiliko makubwa zimeongezeka nchini humo."

Jenerali Haftar amesisitiza ulazima wa kuondolewa vikosi vya wanajeshi wa kigeni nchini Libya na kusema: Iwapo juhudi za kutatua mgogoro wa nchi hiyo kwa njia ya amani zitashindikana, ataingia katika vita vya maamuzi vya kuikomboa nchi hiyo.
Jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa suluhu pekee la mgogoro wa Libya ni kuitishwa uchaguzi wa Bunge na Rais.