Mripuko wa kipindupindu waua mamia ya watu nchini Malawi
(last modified Thu, 10 Nov 2022 10:59:26 GMT )
Nov 10, 2022 10:59 UTC
  • Mripuko wa kipindupindu waua mamia ya watu nchini Malawi

Wizara ya Afya ya Malawi imetangaza habari ya kuaga dunia mamia ya watu kutokana na mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini humo.

Taarifa ya wizara hiyo imesema watu 214 wamepoteza maisha kutoka na maradhi hayo, katika mripuko wa sasa ambao unaripotiwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Umoja wa Mataifa umesema kesi 7,499 za ugonjwa wa kipindupindu zimerekodiwa nchini humo tokea Machi mwaka huu hadi sasa. Hata hivyo, Storm Kabuluzi, Mkurugenzi wa Idara ya Kuzuia Magonjwa kwenye Wizara ya Afya ya Malawi amesema takwimu hizo zinaashiria kupungua kwa maambukizi ya maradhi hayo, baada ya kuongezeka mwezi Oktoba.

Mapema wiki hii, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema kuwa, Malawi imepokea dozi milioni 2.9 za chanjo ya kipindupindu, ili kupiga jeki kampeni ya kukabiliana na mripuko wa sasa ambao awali ulianzia kusini mwa nchi hiyo, lakini sasa umeenea katika mikoa ya kaskazini na katikati ya Malawi.

Uhaba wa maji safi na salama na suhula za matibabu unavyolemaza vita dhidi ya kipindupindu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la WHO na la Kuhudumia Watoto UNICEF yametangaza kuongeza nguvu kwenye juhudi za kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo nchini Malawi.

Licha ya juhudi zinazoendelea katika kukabiliana na mripuko wa kitaifa wa kipindupindu, lakini mapungufu makubwa yameonekana kama uhaba wa vifaa muhimu vya matibabu.

UNICEF na WHO zimetoa wito kwa washirika na wafadhili kusaidia kutoa fedha za ziada na misaada mingine ili kuiwezesha Malawi kukabiliana na changamoto hizi na kudhibiti mripuko huu.