Waasi wa Tigray kuweka silaha chini iwapo askari wa Eritrea wataondoka Ethiopia
Serikali ya Ethiopia na makamanda wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) wameafikiana kuweka silaha chini, mara tu wanajeshi wa nchi jirani ya Eritrea watakapoondoka nchini humo.
Makubaliano hayo ya kuweka silaha chini na kuanisha njia za utekelezaji wa mapatano ya kudumu yaliyofikiwa Afrika Kusini hivi karibuni, yametiwa saini huko Nairobi, mji mkuu wa Kenya jana Jumamosi kwa upatanishi wa Umoja wa Afrika.
Ingawaje wapiganaji wa Tigray hawajaitaja Eritrea kwa njia ya moja kwa moja, lakini makubaliano yaliyosainiwa baina ya Mkuu wa Majeshi ya Ethopia, Field Marshal Birhanu Jula na Luteni Jenerali Tadese Woreda, Kamanda Mkuu wa TPLF yamesema pande mbili hizo zitatambua jeshi moja la Ulinzi la Ethiopia.
Jumatano iliyopita na baada ya miaka miwili ya mzozo kati ya jeshi la Ethiopia na wanamgambo wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray TPLF, pande hizo mbili zilitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano katika mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria.
Mazungumzo kati ya jeshi la Ethiopia na TPLF, yalianza tarehe 25 Oktoba huko Pretoria, mji mkuu wa Afrika Kusini. Mnamo tarehe 5 Oktoba, pande hizo mbili ziliukubali wito wa Umoja wa Afrika wa kufanya mazungumzo ya kutafuta suluhu.
Eneo la Tigray lililoko kaskazini mwa Ethiopia limekuwa likishuhudia mzozo na mapigano kati ya wanamgambo wa kundi la TPLF na jeshi la nchi hiyo tangu Novemba 2020. Idadi kubwa ya raia wameuawa na wengine takribani milioni mbili wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano hayo.