UN: Misaada ya chakula katika eneo la Tigray haiwiani na mahitaji
Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (WFP) umeeleza kuwa, misaada ya chakula inayopelekwa katika eneo la Tigray lililokumbwa na mapigano kaskazini mwa Ethiopia haiwiani na mahitaji yaliyopo licha ya kuanza kutekelezwa mapatano ya kusitisha mapigano.
WFP imeeleza kuwa, shirika hilo na washirika wake wanahitaji haraka kufika kwenye maeneo yote ya Tigray ili kugawa misaada ya chakula na lishe kwa raia milioni 2.3 wanaohitaji msaada. Suala la kurejesha ugawaji wa misaada ya kibinadamu kwa raia wa Tigray ni sehemu muhimu ya mapatano yaliyosainiwa tarehe Pili mwezi huu wa Novemba kwa minajili ya kuhitimisha vita vya miaka miwili ambavyo vimeuwa watu wengi na kusababisha mgogoro wa kibinadamu.
WFP imeeleza kuwa, korido zote nne za barabara zinazoelekea Tigray zimefunguliwa tena tangu baada ya kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita, na ndege za misaada ya kibinadamu sasa zinafanya safari zake katika miji muhimu na hivyo kuruhusu ongezeko kubwa la misaada kulifikia eneo la Tigray. Hata hivyo Shirika la WFP limesema kuwa, imekuwa vigumu kufika katika baadhi ya maeneo ya mashariki na katikati mwa Tigray kwa ajili ya utoaji misaada. Akina mama na watoto wasiopungua 170,000 wanaohitaji msaada wa chakula wameathiriwa na suala hilo.
Hata kabla ya kusitishwa misaada ya kibinadamu huko Tigray Umoja wa Mataifa ulikuwa umetahadharisha kwamba, watu wengi katika eneo hilo tayari wameathiriwa na njaa; ambapo asilimia 90 ya watu milioni sita wa eneo hilo walikuwa wakihitaji misaada ya chakula.