Waasi wa Tigray kusalimisha silaha nzito Jumamosi ijayo
Balozi wa Ethiopia nchini Kenya amesema kuwa kundi la waasi la Tigray People's Liberation Front (TPLF) litasalimisha silaha zake nzito siku ya Jumamosi ijayyo kufuatia mazungumzo kati ya makamanda wakuu wa jeshi na TPLF.
Balozi Bacha Debele alitoa tangazo hilo katika video iliyowekwa kwenye YouTube.
Amesema: “Wapiganaji wa TPLF walitakiwa kuzisalimisha silaha nzito tarehe 17 Novemba, lakini hilo halikutekelezwa; sasa imeamuliwa wazisalimishe tarehe 3 Desemba.”
Bw Bacha alisema makamanda wa vita "wanakutana kila siku" kujadili mchakato wa kupokonya silaha na wapiganaji wa TPLF wanakusanywa katika maeneo maalumu.
Ameongeza kuwa taarifa alizozipata leo zinaonyesha kuwa shughuli zimeanza kuwakusanya wapiganaji wa TPLF katika maeneo yaliyotengwa. Balozi huyo pia amesema itakuwa jambo la aibu kuzungumzia hadharani kuhusu gharama ya binadamu ya vita vya Tigray.
Serikali ya Ethiopia na waasi wa TPLF walitia saini makubaliano ya amani nchini Afrika Kusini mapema mwezi huu ili kumaliza kwa amani vita hivyo vya miaka miwili.
Eneo la Tigray lililoko kaskazini mwa Ethiopia limekuwa likishuhudia mzozo na mapigano kati ya wanamgambo wa kundi la TPLF na jeshi la nchi hiyo tangu Novemba 2020. Idadi kubwa ya raia wameuawa na wengine takribani milioni mbili wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano hayo.